Welcome to F.I.E.L.D.- the First Ismaili Electronic Library and Database.

Mkapa azindua ujenzi wa kituo cha Aga Khan - DAR TO HAVE NEW AGA KHAN SCHOOL LAUNCHED - 2005-03-17

Date: 
Thursday, 2005, March 17
Location: 
Source: 
www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2005/03/18/35023.html IPP Media
mkapa.jpg

Mkapa azindua ujenzi wa kituo cha Aga Khan
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wenye asili ya Asia, wakimsikiliza Rais Benjamin Mkapa na Mgeni wake Aga Khan wakitoa hotuba wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa Ujenzi wa Shule ya wenye vipaji maalum ya Aga Khan Academy Tanzania.

Rais Benjamin Mkapa amezishukuru taasisi binafsi zikiwemo za dini zinazochangia huduma za kijamii zikiwemo za elimu na afya kwa kuinua kiwango cha elimu nchini na kuliongezea taifa hazina ya vyuo vyenye ubora.

Rais Mkapa alisema hayo jana wakati wa sherehe za kuweka Jiwe la Msingi la Kituo Maalum cha taaluma cha wanafunzi wenye vipaji kinachotarajiwa kujengwa, Jijini Dar es Salaam cha Aga Khan Academy.

Akihutubia wananchi waliokwenda kushuhudia sherehe hizo, Rais Mkapa alisema bila msaada wa taasisi hizo katika elimu, malengo ambayo Tanzania imejiwekea hayawezi kufikiwa.

'Napenda kuwashukuru sana watoa elimu binafsi nchini kwa mchango wao wa maana sana wa kuiwezesha serikali kufikia mafanikio katika elimu,' alisema.

Alisema familia ya Aga Khan na jumuiya yake ina historia ndefu katika maendeleo ya elimu ya Tanzania kuanzia mwaka 1896 wakati ilipojenga Kituo mjini Bagamoyo.

Alisema katika miaka ya 60 wakatiTanzania ikielekea kupata Uhuru, shule za Aga Khan nchini zilikuwa 67, kati ya hizo chekechea 11, shule za msingi 52 na shule nne za sekondari.

Rais Mkapa alisema Tanzania imejitahidi kuboresha elimu ya shule za msingi kwa kuongeza uandikishwaji wa wanafunzi wa shule za msingi kutoka asilimia 56 mwaka 1995 kufikia asilimia 90.5, mwaka jana.

Aidha, alisema kiwango cha kufaulu kwa shule za msingi kimepanda kutoka asilimia 20 katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kufikia asilimia 49 kwa mwaka jana.

Alisema kuwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, uandikishwaji wa watoto katika shule za sekondari umeongezeka mara mbili kutoka 176,000 mwaka 1995 na kufikia zaidi ya 500,000 mwaka huu.

Aliongeza kuwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES), uandikishaji wa wanafunzi wa sekondari utakuwa na uwiano wa asiliamia 50 ifikapo mwaka 2010 wakati wanafunzi 500,000 watakuwa wanaingia kidato cha kwanza kwa mwaka.

Alisema mpango huo utabadilisha uandikishwaji wa elimu ya sekondari kutoka kidato cha kwanza hadi cha sita na kufikia watoto milioni 2 ifikapo mwaka 2010 tofauti na watoto 345,000 kwa mwaka 2003.

Kiongozi wa Dini ya Ismailia, Aga Khan, akiongea katika sherehe hizo aliahidi kuwa wanafunzi watakofanya vizuri katika masomo yao, wataingizwa kwenye Kituo hicho na kusomeshwa bure.

'Ni lazima tutoe nafasi ya elimu kwa kiwango cha juu cha kimataifa kwa wanafunzi watakaofanya vizuri zaidi ya wenzao,' alisema Kiongozi huyo.

Alisema kuwa anaamini kuwa nchi zinazoendelea zinahitaji kuendelea kwa nia ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi na viwango vya maisha.

Alisema inasikitisha kuona watu wengi katika nchi zinazoendelea hawapewi nafasi ya kutumia akili zao kwa uwezo wao.

'Ndio maana nilazima tuanzishe taasisi za elimu zitakazo wasaidia kujipima uwezo wao wa kusoma na kufanyakazi katika kiwango cha kimataifa,' alisema.

Akielezea historia ya Aga Khana, Kiongozi huyo alisema hivi sasa Taasisi yao ina mtandao wa zaidi ya shule 300 katika bara la Afrika na Asia, kuanzia shule za msingi hadi elimu ya juu.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa shule za taasisi hiyo zinatoa elimu bora na wote waliopita kwenye shule hizo sio tu wamekuwa na uwezo lakini pia wamekuwa watu muhimu katika kuchangia maendeleo ya jumuiya zao na nchi zao.

Alisema katika kipindi cha miaka kumi ijayo taasisi yake inampango wa kufungua Vituo 19 vya elimu ambavyo vitakuwa bora duniani.

SOURCE: Nipashe


Back to top